19 Juni 2019 - 09:50
Mohammad Morsi azikwa kimya kimya Cairo, Misri

Mwili wa rais wa zamani wa Misri aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia umezikwa huku usalama ukiwa umeimarishwa pakubwa sambamba na familia na wakili wake kushiriki katika mazishi hayo.

(ABNA24.com) Mwili wa rais wa zamani wa Misri aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia umezikwa huku usalama ukiwa umeimarishwa pakubwa sambamba na familia na wakili wake kushiriki katika mazishi hayo.

Mohammad Morsi aliyepinduliwa na jeshi tarehe Tatu mwezi Julai mwaka 2013 alifariki dunia jana wakati kesi iliyokuwa ikimkabili ikisikilizwa, na kuzikwa leo katika makaburi ya Medinat Nasr mashariki mwa Cairo mji mkuu wa nchi hiyo. Mohammad Morsi Issa al Ayyat rais wa Misri aliyepinduliwa na jeshi mashuhuri kwa jina la Mohammad Morsi alifariki dunia jana mahakamani wakati kesi iliyokuwa ikimkabili ya tuhuma za kufanya ujasusi ikiendelea kusikilizwa.

Televisheni ya Msri imetangaza habari ya kuaga dunia Morsi na kuripoti kuwa rais huyo wa zamani wa Misri alipoteza fahamu na kufariki dunia wakati kesi iliyokuwa ikimkabili ikiendelea kusikilizwa. Wakati huo huo Harakati ya Ikhwanul Muslimin ya nchini humo imetoa radiamali yake ya awali kuhusu kifo cha Morsi na kuitaja serikali ya Cairo kuwa mhusika wa kifo hicho ilichokitaja kuwa ni cha makusudi. Shirika la Haki za Binadamu Human Rights Watch  limesema kuwa serikali ya Misri inapasa kubeba dhima kufuatia kifo cha Mohammad Morsi kutokana na serikali hiyo kushindwa kumpatia matibabu aliyopasa kupewa na haki za msingi wakati akiwa jela.



/129